Hivi ndivyo Facebook, WhatsApp ilivyo boreshwa na kuwa na stori sawa na za Snapchat
Facebook imezindua kiungo chake ambacho kinafanana na kiungo cha Stori kwenye Snapchat. Kampuni hiyo inawahamasisha watu kupiga picha kwa wingi na kuzihariri pamoja na kuzirembesha kwa viungo kama vile theluji inayomwagika au upinde wa mvua.
Watu wanaotumia aina ya karibuni zaidi ya programu tumishi ya Facebook wataweza pia kutumia kamera kwenye app hiyo na kutuma picha kwa njia ya faragha kwa marafiki zao au kuichapisha hadharani kwenye ukurasa wao.
Sawa na ilivyo kwenye Snapchat, wanaotumia Facebook sasa wataweza pia kupakia kwenye mtandao huo mkusanyiko wa picha ingawa mkusanyiko huo utatoweka baada ya saa 24.
Instagram, Facebook Messenger na WhatsApp ambazo pia zinamilikiwa na Facebook, pia ziliongezewa kiungo kama hicho majuzi.
Snapchat imesema inataka sana kuangazia kuunda vifaa na mitambo mbalimbali. Kampuni hiyo imesema inataka kufahamika zaidi kama kampuni ya kuunda kamera badala ya kufahamika zaidi kama mtandao wa kijamii.
Facebook, ambayo kwa sasa inatumiwa na watu 1.86 bilioni duniani, imekanusha tuhuma kwamba ilichukua wazo la kamera kutoka kwa Snapchat. Kampuni hiyo inasema ilipata wazo hilo kutoka kwa watu wanaotumia mtandao huo.
No comments